Wednesday, July 3, 2013

Muda wayoyoma kwa rais Morsi wa Misri

Hali ya taharuki imetanda Misri huku makataa iliyotolewa na jeshi kwa rais wa nchi hiyo Mohammed Mosri ikikaribia kufika ukingoni. Kuna taarifa za kutofautiana kuhusu ikiwa jeshi litatoa taarifa punde baada ya muda huo wa masaa 48 aliopewa rais Morsi kutafuta suluhu ya mgogoro huo kutimia. Jeshi linasemekana tayari kudhibiti jengo la televisheni ya taifa. Maafisa wakuu wa serikali wako kwenye mkutano wa dharura nchini Misri, saa chache kabla ya muda wa mwisho ambao jeshi na upinzani zilimpa rais wa nchi hiyo Mohammed Morsi kusuluhisha mgogoro wa kisiasa unaokumba taifa hilo. Jeshi limesema kuwa litaingilia mzozo unaokumba nchi kwa kutoa mpango wake maalum wa kutatua mgogoro huo, ikiwa pande zote mbili hazitaafikiana. Wafuasi na wapinzani wa rais Morsi wanaanza kujitokeza barabarani kwa maandamano kwa siku ya nne tangu kuanza mwishoni mwa wiki jana. Kwa upande wake Rais Mohammed Morsi amesisitiza kwamba yeye ndiye kiongozi halali wa taifa huku maandamano kati ya wapinzani na wafuasi wake yakisababisha vifo zaidi. Kwenye hotuba aliyotoa kwa taifa usiku wa kuamkia leo, Mosri alipinga makataa ya jeshi kutatua mgogoro wa sasa ifikapo Jumanne. Kiongozi huyo amesema hataamrishwa na yeyote na kuwasihi waandamanaji kuweka utulivu. Hata hivyo watu 16 walikufa katika moja wapo ya maandamano ya wafuasi wa Morsi. Awali jeshi lilitoa mpango wa kurejesha taifa katika uthabiti. Stakabathi iliyopatikana na BBC inasema jeshi linapanga kuvunja katiba, kuweka machakato wa uchaguzi mkuu, na kuvunja bunge. Hapo Jumatatu Jeshi lilisema huenda likaingilia kati ikiwa hali haitabadilika. Morsi na wanasiasa walipewa saa 48 kuafikiana.

Mandla ashindwa katika kesi ya makaburi

Mandla ashindwa katika kesi ya makaburi Imebadilishwa: 3 Julai, 2013 - Saa 13:26 GMT Facebook Twitter Google+ Tuma kwa rafiki yako Chapisha .Mjukuu wa Nelson Mandela, Mandla Mandela ameshindwa katika kesi iliyowasilishwa mahakamani dhidi yake kwa tuhuma za kufukua makaburi ya jamaa za familia yake katika mzozo wa makaburi unaokumba familia ya Mandela. Mgogoro huo unahusu maiti za wanawe Mandela watatu ambao Mandla alihamisha na kuwazika karibu na nyumbani kwake zaidi ya miaka miwili iliyopita. Mahakama kuu iliamua kuwa maiti hao lazima warejeshwe katika makaburi yao Jumatano. Mandela anaendelea kuugua hospitalini na haijulikani ikiwa mawakili wa Mandla watakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama. Jamaa za familia ya Mandela waliwasilisha kesi ya uhalifu dhidi ya Mandla kwa kosa la uhalifu. Msemaji wa polisi, Mzukisi Fatyela aliambia BBC kuwa maafisa wa usalama watachunguza tuhuma dhidi ya Mandla za kufukua makaburi kinyume na sheria Inahusisha maiti za watoto watatu wa Mandela ambao inaaminika walifukuliwa na Mandla kutoka makaburi ya familia miaka miwili iliyopita. Familia ya Mandela, inataka kurejesha miili hiyo katika kijiji cha Qunu, ambako Mandela, ambaye anaumwa sana hospitalini anataka kuzikwa akifa. Kesi hiyo iliyosikilizwa katika mahakama kuu ya Mthatha, katika mkoa wa Mashariki iliahirishwa hapo jana lakini hukumu ikitaolewa Jumatano. Wiki jana, mahakama ilitoa amri ya muda kwa maiti za watatu hao kuhamishwa kutoka nyumbani kwa Mandla katika kijiji cha Mvezo hadi Qunu, umbali wa kilomita 22. Lakini Mandla Mandela, ambaye alitawazwa kama kiongozi wa kijamii na babu yake, sasa anapinga vikali amri hiyo.

Msaada wa UK hautumiki vyema Afrika

Malaria imeathiri zaidi bara la Afrika, Serikali ya Uingereza inanuia kupunguza kwa asilimia hamsini idadi ya vifo vinavyotokana na Malaria katika nchi kumi ambazo inasaidia ifikapo mwaka 2015. Mawaziri wa Uingereza wanaonya kuwa vyandarua vinavyokinga dhidi ya Mbu na ambavyo Uingereza imenunua kwa ajili ya nchi hizi havitoshi katika harakati za kuangamiza Malaria. Taarifa zinazohusianaUingereza, afyaUingereza imeweza kununua vyandarua milioni 25, tangu mwaka 2010, lakini wakaguzi wa fedha nchini humo wanasema kuwa matumizi yake hususan kwa watoto wadodgo yanasikitisha, kwani havitumiki sana. Wakaguzi hao wanataka Uingereza kushirikiana na watu wanapokea msaada huo ili kubadili maoni yao kuhusu matumizi ya vyandarua na umuhimu wake na pia kuhakikisha kuwa manufaa yanapatikana kwani pesa zimetumika kuvinunua vyandarua hivyo. Mawaziri wamesema kuwa hatua ya matumizi ya vyandarua kuongezeka ni sehemu ya mpango unaolenga malengo mengi katika kuokoa maisha ya watu. Hadi sasa hakuna chanjo dhidi ya Malaria na ugonjwa huo umesababisha vifo vya watu 660,000, mwaka jana na kuwaacha watu milioni 250 wakiwa wagonjwa sana. Shirika la afya duniani limetahadharisha kuwa huenda ufadhili wa mipango ya kuangamiza Malaria ukapungua licha ya kuwa ugonjwa huo ni janga kubwa duniani na husababisha changamoto za kiuchumi kwa nchi zenye idadi kubwa ya watu wanaougua ugonjwa wenyewe. Uingereza ilitumia pauni milioni 252 kati ya mwaka 2011-2012, katika nchi 18, kati ya hizi 16 zikiwa barani Afrika katika mpango wa kuangamiza Malaria. Bajeti inatarajiwa kupanda hadi pauni milioni 494 kati ya mwaka 2014-2015, na kuifanya Uingereza kuwa mfadhili wa tatu kwa mkubwa kote duniani.

Tuesday, July 2, 2013

Shinikizo zaidi dhidi ya rais Morsi

Maandamano dhidi ya Morsi yamekuwa yakifanyika Misri mara kwa mara Rais wa Misri Mohammed Mosri anaendelea kukabiliwa na shinikizo kali huku maafisa zaidi wa serikali yake wakiendelea kujiuzulu nao waandamanaji wakianza kukusanyika tena katika bustani ya Tahrir. Msemaji wa rais na mwenzake wa baraza la mawaziri nao pia wamejiuzulu , baada ya mawaziri sita kuondoka serikali mwishoni mwa wiki kufuatia maandamano makubwa dhidi ya serikali. Awali taarifa ya rais ilipinga vikali onyo la jeshi dhidi ya utawala wa Morsi kwa kumpa masaa 48 kusuluhisha mgogoro wa kisiasa unaokumba taifa hilo. Chama rasmi cha upinzani National Salvation Front, kimesema kinaunga mkono tamko la jeshi lakini katu hakiungi mkono mapinduzi ya kijeshi. Taarifa hiyo ya rais imesema kuwa hatua hiyo ya jeshi kuingilia kati itazua hali ya suitofahamu zaidi. Jeshi limekanusha madai kuwa makataa hayo ni sawa mapinduzi ya kijeshi. Serikali imesema kuwa Morsi amewasiliana na rais Barack Obama kuhusu hali ya kisiasa inayoshuhudiwa Misri. Wakati huohuo, shirika la habari la kitaifa Misri, limeripoti kuwa waziri wa mambo ya nje Mohamed Kamel Amr amejiuzulu. Ikiwa ombi lake litakubaliwa, atakuwa mmoja wa mawaziri wengine watano ambao wamejiuzulu kufuatia mgogoro huo wa kisiasa. Mnamo jumapili, mamilioni walifanya maandamano wakimtaka rais ajiuzulu. Maandamano mengine makubwa yalishuhudiwa Jumatatu huku ripoti zikisema kuwa watu wanane waliuawa wakati waandamanaji walipovamia makao makuu ya chama tawala cha Muslim Brotherhood. Wapinzani wa Morsi,wanamkosoa kwa kuweka maslahi ya chama mbele huku akiwapuuza wale wasiounga chama hicho. Morsi alichaguliwa kama rais wa kwanza wa kiisilamu katika uchaguzi wa mwezi Juni mwaka 2012 tarehe 30 baada ya kushinda uchaguzi uliotazamiwa na wengi kuwa huru na wa haki baada ya mapinduzi ya kiraia yaliyomwondoa mamlakani Hosni Mubarak

Familia ya Mandela yazozana kuhusu makaburi

Huku rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson Mandela akiendelea kuugua mjini Pretoria, jamaa zake wamejikuta kwenye malumbano kuhusu mgogoro ambao umejitokeza wazi kwenye vyombo vya habari. Badhi ya jamaa za familia wamemshtaki mjukuu mkubwa wa Mandela, Mandla, katika juhudi za kutaka kufukua maiti za wanawe watatu wa Mandela ili wawazike katika makaburi ya Qunu, ambako Mandela anataka azikwe. Na Mgogoro kuhusu kutaka kuwafukua wafu hao ni ishara ya mgawanyiko mkubwa katika familia kubwa ya Mandela, wake zake watatu , watoto sita na wajukuu 17 na vitukuu 12 . Kulingana na baadhi ya viongozi wa kijamii, wakati familia yake inapoendelea kuzozana , roho ya Mandela haiwezi kuwa na amani. Jamaa kumi na sita wa familia ya Mandela pamoja na viongozi wa kijamii wiki jana walipewa idhini ya muda na mahakama kufukua maiti hao na kuwapeleka katika mji wa Qunu, ambako makaazi ya Mandela yapo. Lakini Mandla Mandela, ambaye kulingana na vyombo vya habari, alihamisha maiti hao umbali wa kilomita 22 kutoka mji wa wa Qunu hadi nyumbani kwake eneo la Mvezo mnamo mwaka 2011, anapinga uamuzi huo. Maiti hao ni pamoja na Makgatho Mandela, babake Mandla aliyefariki kutokana na ugonjwa wa ukiwmi, mwaka 2005 pamoja na ndugu zake, Thembekile, aliyefariki katika ajali ya barabarni na mwanawe wa kwanza aliyefariki akiwa na miezi tisa, walizikwa kwenye makaburi yaliyokaribiana. Mamia wamekuwa wakikesha kumuombea Mandela apate nafuu Watatu hao walifukuliwa bila ya idhini ya familia yote ya Mandela na viongozi wa kijamii wa ukoo wa AbaThembu ambao pia ni ukoo wa Mandela. Wanaamini kuwa roho ya Mandela, ina sumbuka hivi sasa kutokana na mzozo kwenye familia yake na ndio maana roho yake haikatiki. Watu kumi na sita ni mashahidi katika kesi ya kuomba mahakama idhini ya kufukua maiti hao, akiwemo mkewe Mandela, Graca Machel, mwanawe Mandela Makaziwe na viongozi wakuu wa ukoo wa AbaThembu. Kinachohojiwa zaidi kwenye mzozo huu ni nani atachukua nafasi ya Mandela kama kiongozi wa familia? Viongozi wa kijamii walimteua Mandla kama kijana mwenye umri mkubwa zaidi kuweza kuchukua nafasi ya Mandela, na kumkabidhi jukumu la chifu Zwelivelile wa ukoo wa Thembu. Pia ni mbunge katika chama tawala ANC. Lakini wengi katika familia wanaonekana kutopendezwa na miendeno yake, akiwemo Makaziwe, mwanawe Mandela wa kike. Mpango wake wa kutaka kufungua makavazi katika shamba ambalo makaburi hayo yapo, imewaacha wengi vinywa wazi katika familia hiyo. Katika mgogoro mwingine, wanawe wa kike na wakubwa wa Mandela, Makaziwe na Zenani wameenda mahakamani wakitaka kuwanondoa wasaidizi watatu wa Mandela kutoka katika kampuni za baba yao. Wawili hao wanataka umiliki wa kampuni hizo ambazo ni za thamani ya mamilioni ya dola. Mjukuu mkubwa wa Mandela , Mandla Mandela wiki jana aliandaa mkutano wa dharura wa kijamii ambapo inasemekana Mandla alilaaniwa vikali kwa kuhamisha maiti za jamaa zake bila idhini. Baadhi wanaamini kuwa Mandela lazima asuluhishe mzozo huu kabla ya ya kifo chake. Moja ya imani za kitamaduni nchini Afrika Kusini ni kuwa mtu huwa hafi wakati ana mambo yanayomsubiri kuyasuluhisha. Baadhi wanaamini kuwa badhi ya mambo ambayo bado hajakamilika kwa Mandela ni kuweza kusuluhisha migogoro hii ndani ya familia pamoja na kuipatanisha familia take. Mandela alistahili kuafikiana na familia yake kabla ya kufukua miili za jamaa zake. Wajumbe wa ukoo wa AbaThembu, wameandaa mkutano wa dharura mjini Qunu baadaye mwezi huu kusuluhisha mizozo hiyo.

Sherehe za siku ya kuzaliwa Mandela kupangwa

Wananchi wa Afrika Kusini wanamuombea Mandela aliyelazwa hospitalini. Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ameambia taifa hilo lianze kujiandaa kwa sherehe ya siku ya kuzaliwa ya Mandela tarehe 18 mwezi Julai. Mandela ambaye anaheshimika sana kote duniani, atafikisha umri wa miaka 95,lakini kwa sasa angali mahututi hospitalini mjini Pretoria. Alilazwa hospitalini tarehe 8 mwezi Juni akiwa na maradhi ya mapafu. Kauli ya Zuma inakuja baada ya mke wa zamani wa Mandela Winnie Mandela, kukashifu chama ha ANC kwa kumnasa kwa video Mandela, walipomtembelea kwake nyumbani mwezi Aprili. Kanda hiyo ilionyesha Mandela akiwa na mshangao na bila ya tabasamu wakati wa ziara ya mmoja wa vigogo wa ANC nyumbani kwake. Winnie Madikizela-Mandela, alisema "kweli siwezi kueleza ambavyo familia ilihisi uchungu kuhusiana na kanda hiyo, na haikupaswa kwa jambo hilo kufanyika.'' Ikijibu tuhuma hizo, chama cha ANC kilitetea ziara hiyo, kikisema kuwa haikuwa na njama ya kutaka kujitafutia umaarufu. Hapo Jumatatu, rais alitoa taarifa kusema kuwa wananchi wa Afrika Kusini waanze kujiandaa kwa sherehe za kuzaliwa kwa Madiba. "lazima sote tufanye angalau jambo zuri kwa sababu ya utu kwa siku hiyo kama ujumbe wetu mzuri kwa Mandela,'' alisema Zuma. Mandela anasifiwa sana kwa kuongoza vita dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi, nchini Afrika Kusini na kisha kuhubiri maridhiano licha ya kufungwa jela kwa miaka 27. Alituzwa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1993 na kisha kuchaguliwa kama rais mwaka uliofuata. Aliondoka mamlakani mwaka 1999 baada ya kutawala kwa muhula mmoja.

Waathiriwa wa mashambulizi ya 1998 wakumbukwa TZ

Rais wa Marekani Barack Obama ameweka maua kwenye makaburi ya waathiriwa wa mashambulizi ya mabomu dhidi ya ubalozi wa Marekani nchini Tanzania mwaka 1998, kama ishara ya kuwakumbuka. Raia 11 wamarekani waliuawa katika shambulizi hilo lililofanywa na kundi la kigaidi la al-Qaeda ambaklo lilifanyika wakati mmoja na shambulizi lililofanywa dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Nairobi, Kenya. Obama aliuungana na rais mstaafu wa Marekani George W Bush kwa kumbukumbu hizo. Rais Obama yuko katika mkondo wa mwisho wa ziara yake ya pili ya Afrika akiwa rais , ambapo alitembelea Senegal na Afrika Kusini. Aidha Obama pia atamtembelea kituo cha kuzalishha umeme kinachomilikiwa na Marekani nchini humo, kufuatia tangazo lake mwishoni mwa wiki la mradi wa umeme utakaogharimu mabilioni ya dola. Mradi huo wa miaka mitano, unatarajiwa kusaidia kuongeza kasi ya uzalishaji wa umeme kusini mwa jangwa la Sahara,kwa ushirikiano na mataifa ya kiafrika pamoja na sekta binafsi. Akiwa nchini humo, Obama pia anatarajiwa kuzindua mpango unaonuia kusaidia nchi za Afrika Mashariki ikiwemo, Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda kushirikiana kibiashara. Wakati huohuo, mkewe Obama, Michelle anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa wake za marais, unaoandaliwa na taasisi ya George W Bush huku ukiongozwa na mkewe Laura Bush.

Rais wa zamani wa Chad akamatwa Senegal

Polisi nchini Senegal , wamemkamata rais wa zamani wa Chad, Hissene Habre, aliyekuwa anatafutwa kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa utawala wake wa miaka 8. Wakili wa Bwana Habre, El Hadji Diouf, alisema kuwa alikamatwa na polisi kutoka nyumbani kwake mjini Dakar na kupelekwa sehemu isiyojulikana. Habre mwenye umri wa miaka 70, amekuwa akitumikia kifungo cha nyumbani, nchini Senegal tangu mwaka 2005 alikokimbilia baada ya kung'olewa mamlakani mwaka 1990. Aanatuhumiwa kuwatesa maelfu ya watu, wanaominika kuwa wapinzani wake. Mwaka jana mahakama ya kimataifa ya haki, iliamuru Seengal kumchukuliwa hatua za kisheria au kupeleka kwingineko ambako atakabiliwa na sheria kwa uhalifu aliotenda. Kukamatwa kwake kunakuja siku kadhaa baada ya rais wa Marekani, Barack Obama kumsifu rais Macky Sall kwa hatua zake za kuelekea katika kumfungulia mashtaka Habre mwanzoni mwa ziara yake ya Afrika. Mashirika ya kutetea haki za binadamu, yamekuwa yakishinikiza Senegal kwa miaka mingi, kumfungulia mashtaka Habre. Tuhuma anazokabiliwa nazo ni za tangu mwaka 1982, wakati alipoingia mamlakani hadi mwaka 1990 alipoondolewa uongozini kwa njia ya mageuzi . Habre alishtakiwa kwa mara ya kwanza nchini Senegal mwaka 2000, lakini mahakama za nchi hiyo ikaamua kuwa wakati huo isingeweza kushtakiwa huko. Waathiriwa wa utawala wake baadaye waliwasilisha malalamishi chini ya sheria ya kimataifa ya Ubelgiji ambayo inaruhusu majaji wake kusikiliza na kuhukumu washukiwa wa kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu kokote duniani. Hata hivyo Senegal imekataa ombi la Ubelgiji kumhamisha nchini humo ili ahukumiwe.