Tuesday, July 2, 2013
Rais wa zamani wa Chad akamatwa Senegal
Polisi nchini Senegal , wamemkamata rais wa zamani wa Chad, Hissene Habre, aliyekuwa anatafutwa kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa utawala wake wa miaka 8.
Wakili wa Bwana Habre, El Hadji Diouf, alisema kuwa alikamatwa na polisi kutoka nyumbani kwake mjini Dakar na kupelekwa sehemu isiyojulikana.
Habre mwenye umri wa miaka 70, amekuwa akitumikia kifungo cha nyumbani, nchini Senegal tangu mwaka 2005 alikokimbilia baada ya kung'olewa mamlakani mwaka 1990.
Aanatuhumiwa kuwatesa maelfu ya watu, wanaominika kuwa wapinzani wake.
Mwaka jana mahakama ya kimataifa ya haki, iliamuru Seengal kumchukuliwa hatua za kisheria au kupeleka kwingineko ambako atakabiliwa na sheria kwa uhalifu aliotenda.
Kukamatwa kwake kunakuja siku kadhaa baada ya rais wa Marekani, Barack Obama kumsifu rais Macky Sall kwa hatua zake za kuelekea katika kumfungulia mashtaka Habre mwanzoni mwa ziara yake ya Afrika.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu, yamekuwa yakishinikiza Senegal kwa miaka mingi, kumfungulia mashtaka Habre.
Tuhuma anazokabiliwa nazo ni za tangu mwaka 1982, wakati alipoingia mamlakani hadi mwaka 1990 alipoondolewa uongozini kwa njia ya mageuzi .
Habre alishtakiwa kwa mara ya kwanza nchini Senegal mwaka 2000, lakini mahakama za nchi hiyo ikaamua kuwa wakati huo isingeweza kushtakiwa huko.
Waathiriwa wa utawala wake baadaye waliwasilisha malalamishi chini ya sheria ya kimataifa ya Ubelgiji ambayo inaruhusu majaji wake kusikiliza na kuhukumu washukiwa wa kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu kokote duniani.
Hata hivyo Senegal imekataa ombi la Ubelgiji kumhamisha nchini humo ili ahukumiwe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment