Uganda imetangaza kuweka kodi ya 10% kwa pesa zote zinazotumwa kwa njia ya simu na mbinu zingine za kutuma pesa.
Hii itaathiri pesa zinazotumwa na Waganda
waishio nchi za ng'ambo. Waziri wa fedha Maria Kiwanuka pia amesema kuwa
anapanga kukusanya zaidi ya $16.5m (£10.6m) kwa kutoza kodi simu zote za
kimataifa kutoka nchini humo.Mwandishi wa BBC mjini Kampala , anasema kuwa wengi wanahofia kuwa bajeti hii, iliyosomwa Alhamisi, inawalemea zaidi watu maskini katika jamii.
Waziri Kiwanuka aliambia bunge kuwa zaidi ya $767m zilizokusanywa na serikali mwaka uliopita zilitoka kwa Waganda waishio ngambo.
Kwa mujibu wa gazeti huru nchini Uganda, Daily Monitor, ushuru huo mpya unaotozwa pesa zinazotumwa kwa simu za mkononi utaathiri zaidi ya watumiaji 8.9m wanaotumia mitandao sita ya simu nchini Uganda.
Imeripoti pia kuwa serikali inanuia kukusanya takriban $12m kwa mwaka.
Huduma hii ya kutuma pesa kwa njia ya simu ni maarufu sana nchini Uganda ikizingatiwa kuwa raia wengi wa nchi hiyo hawana akaunti za benki.
Huhduma hii hutumiwa kuwatumia jamaa pesa nyumbani au hata kulipia madeni.
Hii bajeti sio juu ya kuweka kodi mpya, ni kukusanya tu kile ambacho hakijachukuliwa kwa muda, alisema waziri huyo.
Kwa upande wake David Holliday, mkurugenzi mtendaji wa shirika la mawasiliano la Telecom, alisema kodi hii mpya bila shaka itaongeza gharama ya matumizi ya simu.
'' pesa kwenye simu imekuwa hali ya maisha ya wananchi wetu kwasababu inamaanisha kuwa hawana haja tena ya kubeba pesa taslimu.
Hata wale ambao hawakuweka pesa zao Benki sasa waliweza kuhifadhi kwenye simu zao kwasababu ni rahisi na bei nafuu'' gazeti la Daily monitor limemnukuu.
Naye Bi Kiwanuka anasema kuwa lengo la bajeti hiyo ni kuwanasa wale ambao hukwepa kulipa kodi na kuishinikiza halmashauri ya ukusanyaji ushuru kufikia malengo ya kodi ya serikali kamilifu.
No comments:
Post a Comment