Tuesday, June 18, 2013

Kesi ya Saif al-Islam kuanza Agosti

 

Islam alionekana na wengi kama mrithi wa babake kabla ya kuuawa kwake.
 
Kesi dhidi ya mwanawe hayati Muamar Gadaffi, Saif al-Islam Gaddafi, itaanza kusikilizwa mwezi Agosti , kwa mujibu wa mwendesha mkuu wa mashtaka nchini Libya.
Inaarifiwa kuwa kesi dhidi ya Saif na maafisa wengine wakuu wa uliokuwa utawala wa Gaddafi, watashtakiwa kwa makosa ya kuunda makundi ya wahalifu , kuchochea ubakaji na kuwafunga watu kinyume na sheria.
Waziri mkuu Ali Zeidan aliambia BBC kuwa watatendewa haki katika kesi zao.
Libya imekataa ombi la mahakama ya ICC iweze kukabidhiwa Saif al-Islam, ili iendeshe kesi yake katika mahakama ya Hague.
Anatakiwa na ICC kwa makosa ya uhalifu wa kivita lakini Libya inasisitiza kuwa kesi yake itaendeshwa nchini humo ambako huenda akakabiliwa na hukumu ya kifo.

Miongoni mwa wale wanaotarajiwa kufikishwa mahakamani ni aliyekuwa mkuu wa ujasusi chini ya utawala wa Kanali Gaddafi Abdullah al-Senussi na waziri mkuu wa zamani al-Baghdadi al-Mahmoudi.
Kwa sasa Saif al-Islam anazuiliwa mjini Zintan , Magharibi mwa Libya, kufuatia kukamatwa kwake na wapiganaji wa kiisilamu mwaka
2011.
                    
Alionekana na wengi kama mrithi wa Kanali Gaddafi, kabla ya kuong'olewa mamlakani kwa Gaddafi mwenyewe miaka miwili iliyopita.
Mwezi Januari Saif al-Islam Gaddafi alifikishwa makahamani mjini Zintan kuhusiana na makosa tofauti ya tuhuma za kuuza habari ambazo zinahatarisha usalama wa kitaifa Libya
Hata hivyo kesi hiyo iliakhirishwa baadaye.

No comments:

Post a Comment