Saturday, May 25, 2013

Sudan Kusini haitashirikiana na mahakama ya ICC

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa mwito kwa bara la Afrika kusimama kidete na kwa umoja, kujiamulia maswala yake yenyewe.                      

 Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir  na rais wa Kenya  Uhuru Kenyatta, mjini Juba, Mei 23, 2013.
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, mjini Juba, Mei 23, 2013.
                       
Rais wa Sudan Salva Kiir amesema Alhamis kuwa kamwe hatakubali kuingia katika mkataba wa mahakama ya uhalifu wa kivita-ICC. Bw. Kiir alikuwa akizungumza baada ya kutembelewa na rais mpya wa Kenya, Bw. Uhuru Kenyatta aliyeahidi kuunga mkono ujenzi wa barabara, njia za reli na mabomba ya mafuta, ili kuboresha mahusiano ya kiuchumi kati ya Kenya na taifa hilo jipya.

Hii ilikuwa ziara ya kwanza kwa rais Uhuru Kenyatta huko Sudan Kusini tangu alipoapishwa kuwa rais wa Kenya na alikaribishwa kama ndugu na rais Kiir aliyemweleza ajihisi kuwa nyumbani.

Rais Kiir aliahidi kusimama wima na kiongozi wa Kenya na wananchi wa Kenya. Bw. Kenyatta alichukua madaraka baada ya kushinda uchaguzi wa kiti cha urais mwezi Machi, wakati huo akiwa bado anakabiliwa na kesi katika mahakama ya ICC, inayomshtumu kwamba alichochea ghasia za uchaguzi  wa mwaka wa 2007.

Lakini huku mataifa ya Magharibi yakisita kumpongeza kufuatia ushindi wake, viongozi wengi wa Afrika walimpongeza na kuahidi kumuunga mkono kwa hali na mali bila kujali mashtaka ya mahakama ya The Hague.

Alhamis rais Kiir aliipuzilia mbali mahakama hiyo ya ICC na kusema Sudan Kusini haina nia ya kutia saini mkataba wa  kushirikiana nayo na hivyo kuchukua msimamo sawa na wa viongozi wengine wengi wa bara la  Afrika wanaosema mahakama hiyo inalenga waafrika. Alisema jamii ya kimataifa imekuwa ikiirai nchi yake kutia saini mkataba na ICC ili ipewe msaada lakini wamesema kamwe hawakubali.

Bw. Kiir alisema viongozi wa Afrika watajadilia  zaidi swala la Kenya na ICC katika mkutano wa mwishoni mwa wiki wakati wa kongamano kuu la Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia wakati wa maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa shirika hilo la Umoja wa Afrika. Alisema viongozi wa Afrika watanena kwa sauti moja na kusimama wima na ndugu na dada zao wa Kenya.

Katika hotuba yake rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alitoa mwito kwa bara la Afrika kusimama kidete na kwa umoja, kujiamulia maswala yake yenyewe.

No comments:

Post a Comment