Takriban mtu mmoja
amekufa kwenye mlipuko wa bomu Jumapili ya leo asubuhi katika kanisa Katoliki
la Olasiti nje kidogo ya mji wa Arusha, Tanzania.
Wengine kadhaa walijeruhiwa huku
balozi wa papa na watawa waliokuwa katika shughuli hiyo maalumu ya
kuzindua parokia mpya ya mtakatifu Yosefu walinusurika.
Kwa mujibu wa Padri Festus Mangwangi ambaye ni paroko msaidizi wa kanisa katoliki jimbo la Arusha, mripuko ulipotokea walikuwa tayari kubariki maji kwa ajili ya uzinduzi wa kanisa, shughuli iliyokuwa ikiongozwa na balozi wa Papa Francis.
Hata hivyo Padre Mangwangi ameiambia BBC kuwa taarifa walizonazo muda mfupi baada ya majeruhi kukimbizwa hospitali, kuna watu watatu kati yao waliofariki na wengine wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Mount Meru mjini Arusha.
Taarifa moja inasema watu zaidi ya 30 walijeruhiwa.
Watalaalamu wa milipuko na polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na mlipuko huo.
Bado hakuna taarifa ya chanzo cha mlipuko au kama kuna mtu au kundi lilohusika.
Lakini msemaji wa polisi alieleza kwamba wanashuku kuwa mlipuko ulisababishwa na bomu.
Hili ni shambaulio la kwanza la bomu nchini Tanzania japokuwa mwaka huu pia kulikuwa na tukio la mauaji ya Padre wa kanisa hilo visiwani Zanzibar, ambaye alipigwa risasi wakati akiwa anajiandaa kuingia kanisani.
No comments:
Post a Comment